Manchester City kukipiga na Arsenal Kombe la Ngao ya Jamii, unachohitaji kujua

Francis Ngala
4 Min Read

Agosti 6 Manchester City na Arsenal zitapepetana kwenye dimba la Wembley nchini Uingereza.

Pambano la Ngao ya Jamii ndilo utangulizi wa kufunguliwa pazia la ligi kuu ya EPL nchini Uingereza kwa msimu mpya wa 2023-2024.

KWANINI MAN CITY NA ARSENAL ?

Pambano la Ngao ya Jamii linazipambanisha bingwa wa ligi kuu nchini Uingereza na mshindi wa kombe la FA wa msimu uliopita 2022/23, lakini kwa vile bingwa alikuwa Manchester City ambao ndio vinara wa ligi kuu ya EPL, Kanuni inasema iliyoshiriki nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ndio itanyukana na bingwa wake kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii.

 HASIRA YA ARSENAL

Vijana wa Mikel Arteta wanakwenda kwenye mchuano huu wakiwa wamejawa na hasira nyingi. Kwanza wanakumbuka vipigo vitatu msimu uliopita katika michezo miwili ya ligi na mmoja wa FA dhidi ya Man City. Pili Arsenal inakumbuka tukio la kubanduliwa kileleni mwa ligi karibu na mwisho wa msimu baada ya kukaa pale juu kwa zaidi ya mechi 20. Ni chachu ya uzito wa mechi hiyo.

VITA VYA MAKOCHA

Mikel Arteta ana kibarua kigumu sana kuipa Arsenal ushindi mbele ya Manchester City. Pep Guardiola ana kibarua kigumu kutetea ubabe wake mbele ya Arsenal.

Makocha wote wawili wanafahamu uzito wa mchezo unaozikutanisha timu hizo. Kwa vyovyote mechi hii itakuwa na presha kubwa, ubabe, ufundi na maarifa ya kutosha kutoka kwa makocha hao.

Ni mifumo gani itawafaa kuibuka na ushindi kati ya iliyomo ? hilo litajibiwa katika mchezo husika.

Ikumbukwe kwamba chini ya mkufunzi Pep Guardiola, Manchester City wameshinda mechi 16 kati ya 19 walizocheza dhidi ya Arsenal, ikijumuisha kila mechi saba zilizopita kwa jumla ya mabao 21-4.

Manchester City ni mabingwa wa ligi msimu uliopita: Picha – The Sun

Walakini, ushindi mara mbili pekee wa Arsenal dhidi ya vijana wa Pep Guardiola umepatikana kwenye Uwanja wa Wembley, ambao umetokea katika nusu fainali ya Kombe la FA mnamo mwaka wa 2017 na 2020. Zaidi ya yote ni matumaini tu kwa Arsenal Jumapili hii.

Ama kweli, ni wakati mzuri sana kuwa shabiki wa Arsenal, kwani ujio wa Kiungo Declan Rice, Jurriën Timber na Kai Havertz unaongeza nguvu kwenye kikosi kilichoisakama City hadi mwisho wa mbio za ubingwa msimu uliopita.

Wakati huo huo, Klabu ya Manchester City imeongeza kiungo wa Croatia Mateo Kovacic na wanaenda katika mchezo huu wakiwa katika kiwango cha juu zaidi kuliko Arsenal na bado wanaingia kwenye msimu ujao kama timu ambayo imebashiriwa kutwaa taji hilo tena na ikiwa watafanya hivyo basi City watakuwa timu ya kwanza katika historia ya ligi kuu ya Uingereza kushinda ligi hiyo mara nne mfululizo.

Kevin De Bruyne ana historia nzuri dhidi ya timu ya Arsenal: Picha – De Bruyne

Manchester City huenda wakaingia uwanjani bila nyota wao Kevin De Bruyne na beki wa kushoto Nathan Ake ambao hawakushirikishwa katika mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Bayern Munich wiki iliyopita kutokana na majeraha.

De Bruyne amefunga magoli sita na kusaidia mawili katika mechi nane alizocheza na klabu ya Arsenal kwenye michezo yote.

Vile vile Arsenal watamkosa Gabriel Jesus ambaye anatarajiwa kukosekana katika mechi za mwanzo wa msimu ujao kutokana na jeraha.

Timu zote mbili zitakuwa katika kiwango bora katika mechi yao ya kwanza ya ushindani msimu huu, na fomu yao ya mwisho wa msimu uliopita inaweza bure ikizingatiwa mapumziko ambayo yanaendelea kukamilika.

 

 

 

 

 

 

Share This Article
Follow:
I am Versatile Multimedia Journalist with years of experience in Digital platforms, Live TV and Radio. In another world am a News Anchor and Reporter.
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *