Wizara ya Afya imefanya mkutano wa mashauriano na Chama cha Madaktari (KMPDU) na kile cha Maafisa wa Kiliniki (KUCO) kuhusiana na malipo ya madaktari wanagenzi.
Mashauriano hayo yalihudhuriwa na Katibu Mkuu wa KMPDU Dkt. Davji Atellah na yule wa KUCO George Gibore miongoni mwa maafisa wengine wa vyama hivyo.
Mazungumzo kuhusu ni pesa ngapi watakazolipwa kila mwezi madaktari na maafisa wa kliniki wanagenzi yamepangwa kuanza Alhamisi wiki ijayo.
Wakati wa mashauriano ya leo Ijumaa, ilikubaliwa kuwa masharti ya malipo ya madaktari na maafisa wa kliniki wanagenzi yapitiwe upya.
“Tukubaliana kujadiliana upya masharti ya malipo yaliyotolewa na Tume ya Mishahara na Marupurupu, SRC,” kilisema chama cha KUCO katika taarifa baada ya kukamilika kwa mkutano huo.
“Maafisa wa kiliniki wanagenzi walio na stashahada watalipwa kulingana na mikataba yao.”
Serikali imekuwa hususan ikivutana na chama cha KMPDU kuhusiana na malipo ya madaktari wanagenzi.
Wakati wa enzi ya Susan Nakhumicha kama Waziri wa Afya, serikali ilipendekeza madaktari kulipwa shilingi elfu 70 kwa mwezi, pendekezo ambalo lilipingwa vikali na KMPDU.
Chama hicho kinataka madaktari hao walipwe shilingi 206,000 kwa mwezi kama ilivyokubaliwa awali katika Mkataba wa Maelewano.
Mahakama imezielekeza pande zote kwenye mzozo huo kufanya majadiliano upya kwa lengo la kusuluhisha vuta ni kuvute hiyo ambayo awali ilisababisha mgomo wa madaktari uliotatiza utoaji wa matibabu katika hospitali za umma kote nchini.