Mwanauchumi na profesa maarufu wa Mali amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela, kwa ukosoaji wake dhidi ya utawala wa kijeshi.
Étienne Fakaba Sissoko pia aliamriwa kulipa faini ya dola 4,900 za Kimarekani.
Msomi huyo mwenye umri wa miaka 41, ambaye amekuwa kizuizini tangu Machi, alishtakiwa kwa kukashifu na kuharibu sifa ya serikali kwa kusambaza habari ghushi.
Mashtaka hayo yanahusiana na kitabu alichochapisha mwaka jana, ambacho alikitetea mahakamani, akisema kazi hiyo ilitokana na ukweli.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema kesi yake ni ya hivi punde zaidi katika ukandamizaji ulioenea dhidi ya wakosoaji na wapinzani wa kisiasa wa watawala hao wa kijeshi.
Waliingia madarakani mnamo Agosti 2020 wakati Rais wa wakati huo Ibrahim Boubacar Keïta alipoondolewa katika mapinduzi baada ya maandamano makubwa ya kuipinga serikali kuhusu jinsi alivyoshughulikia machafuko ya wanajihadi.