Malalah awakemea wanaohujumu maendeleo, awataja kuwa maadui

Martin Mwanje
2 Min Read

Katibu Mkuu wa chama cha UDA Cleophas Malalah amewashutumu watu wanaotatiza utekelezaji wa miradi ya maendeleo unaofanywa na serikali ya Kenya Kwanza. 

Watu kadhaa akiwemo Seneta wa kaunti ya Busia Okiya Omtatah na chama cha wanasheria, LSK chini ya uongozi wa Eric Theuri wameelekea mahakamani kupinga utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na mpango wa nyumba za gharama nafuu.

Malalah anasema watu kama hao ni adui wa maendeleo na wanapaswa kukemewa.

Kulingana naye, Rais William Ruto alichukua hatamu za uongozi kwa ahadi siyo tu ya kuheshimu utawala wa sheria, kuimarisha afisi za kikatiba na afisi huru, bali pia kuinua viwango vya maisha vya Wakenya kupitia utekelezaji wa Ajenda ya Mabadiliko ya Kiuchumi kuanzia Chini hadi Juu, BETA.

“Yeyote, ambaye anachelewesha au kuhujumu utekelezaji wa miradi hii ya maendeleo anapaswa kuchukuliwa kama adui wa maendeleo na kukemewa,” alisema Malalah katika taarifa iliyounga mkono matamshi ya Rais William Ruto kuwa maafisa wafisadi katika idara ya mahakama wanapaswa kuchukuliwa hatua kali.

“Hii inajumuisha wanaowasilisha kesi na maafisa wa idara ya mahakama wanaodhani wanashikilia nyadhifa za juu kuliko mamilioni ya Wakenya waliompa Rais Ruto mamlaka ya kuongoza serikali ili kuwakomboa kutoka hali ngumu iliyowakabili iliyosababishwa na utawala uliopita.”

Katika taarifa, Seneta huyo wa zamani wa kaunti ya Kakamega anasema majaji wafisadi  hawapaswi kujificha nyuma ya uhuru wa mahakama kutumiwa na watu wenye nia ya kuhujumu miradi mbalimbali ya serikali yenye manufaa kwa Wakenya.

Rais William Ruto ameapa kuwa hataruhusu mahakama kutumiwa na watu fulani kuhujumu miradi ya serikali kama vile mpango wa nyumba za gharama nafuu na afya kwa wote.

Ni matamshi ambayo yameshutumiwa vikali na taasisi mbalimbali ikiwemo Tume ya Huduma za Mahakama, JSC na chama cha wanasheria, LSK zinazoonyakuwa matamshi kama hayo huenda yakafanya asasi hiyo muhimu yenye jukumu la kuhakikisha haki inatendeka ikakosa kuheshimiwa.

Website |  + posts
Share This Article