Makamu wa Rais wa Malawi athibitishwa kufariki

Martin Mwanje
2 Min Read

Makamu wa Rais wa Malawi Dkt. Saulos Chilima na watu wengine tisa wamethibitishwa kufariki katika ajali ya ndege. 

Vifo vya 10 hao vimethibitishwa na Rais wa nchi hiyo Dkt. Lazarus Chakwera wakati akiwahutubia wanahabari leo Jumanne.

Ndege hiyo ya kijeshi walimokuwa wakisafaria waathiriwa ilitoweka jana Jumatatu asubuhi.

Ndege hiyo ilipatikana katika mlima Chikangawa ikiwa imeharibika kabisa.

Rais Chakwera ameelezea kusikitikia mno ajali hiyo ambayo awali alisema ilitokana na hali mbaya ya hewa.

Shughuli ya utafutaji imekuwa ikiendelea zaidi ya saa 24 baada ya kutokea kwa ajali hiyo.

Dkt. Chakwera alikuwa ameliagiza jeshi la nchi hiyo kufanya kila liwezalo kuhakikisha ndege hiyo inapatikana na kuelezea imani manusura wangepatikana.

Imani ambayo sasa imemtoweka baada ya kuthibitisha vifo vya watu wote 10 waliokuwa kwenye ndege hiyo, akiwemo makamu wake.

Katika hotuba yake, Rais huyo alisema Kamanda wa Jeshi la nchi hiyo alimtaarifu kuwa ndege hiyo imepatikana ingawa iliharibika kabisa.

Dkt. Chakwera amemwelezea makamu wake na watu wengine waliokuwa kwenye ndege hiyo kama watu wazalendo walioitumikia Malawi kwa bidii ya mchwa.

Nchini Kenya, Kifo chake kinaibua kumbukumbu za Mkuu wa Jeshi Francis Ogolla aliyefariki katika ajali sawia.

Nchini Iran, Rais wa nchi hiyo Ebrahim Raisi pia alifariki katika hali sawia wiki chache zilizopita katika hatua ambayo yamkini itaibua mashaka ya usafiri wa anga kwa kutumia ndege za kijeshi.

 

 

 

 

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *