Makamu wa Rais Tanzania aonekana hadharani baada ya muda mrefu

Marion Bosire
1 Min Read
Daktari Mpango akifuatilia misa akiwa na wajukuu wake

Makamu wa Rais nchini Tanzania Daktari Phillip Isdor Mpango ameonekana hadharani leo Jumapili Disemba 10, 2023 kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu.

Daktari Mpango alihudhuria ibada ya leo katika kanisa katoliki la Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska katika uwanja wa ndege wa Dodoma.

Akizungumza kanisani humo, kiongozi huyo alisema kwamba yeye yuko hai, buheri wa afya kinyume na maneno ambayo yamekuwa yakisambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Kwa siku kadhaa watu wamekuwa wakichapisha picha za makamu huyo wa rais wa Tanzania kwenye mitandao wakitangaza kifo chake.

Kutokana na hilo, Mpango amehimiza watu wa Tanzania kutumia mitandao ya kijamii kwa mambo yenye manufaa kwao na kwa kumwogopa mwenyezi Mungu.

Alielezea kwamba alikuwa nje ya Tanzania kwa muda wa mwezi mmoja kwa shughuli rasmi na sasa amerejea nchini humo.

“Kazi ambayo Mungu alinituma kuifanya sijaimaliza. Wakati utakapofika nitarejea kwa muumba wangu.” alisema Dakta Mpango huku akishukuru wote waliomsemea dua.

Alinukuu kifungu cha Biblia ambacho ni Zaburi 118:17 kinachosema “Sitakufa, bali nitaishi, na kusimulia matendo ya Mwenyezi-Mungu.”

Share This Article