Hatima ya endapo Naibu Rais Rigathi Gachagua atafika mbele ya bunge la Seneti kesho, ili kujitetea itaabainika mapema leo mahakamani.
Jopo la Majaji watatu linakutana kuanzia saa mbili asubuhi kuamua kesi iliyowasilishwa na Gachagua, ya kutaka mahakama imzuie kupitia meno ya Maseneta kujitetea dhidi ya kutimuliwa afisini.
Ni kesi ya pili na ya mwisho kuhusu swala hilo baada ya Jaji Chacha Mwita kukataa abadan hapo jana, kumzuia Naibu Rais kujitetea katika bunge la Seneti.
Kesi ya Gachagua aliyeng’atuliwa afisini na bunge la kitaifa wiki jana itaanza kusikizwa leo na Bunge la Seneti, kabla yake kufika bungeni kesho kujitetea na hatimaye uamuzi kutolewa kupitia kwa kura ya Maseneta kwa kila shtaka kati ya mashtaka yote 11 yaliyowasilishwa dhidi yake.
Endapo Maseneta watamfurusha, Gachagua atakuwa Naibu Rais wa kwanza nchini Kenya kung’olewa afisini na pia afisa wa kwanza wa ngazi za juu serikalini.