Maina Njenga aondolewa mashtaka

Marion Bosire
2 Min Read
Maina Njenga

Aliyekuwa kiongozi wa kundi haramu la Mungiki Maina Njenga sasa yuko huru baada ya afisi ya mkurugenzi wa madhtaka ya umma DPP kuondoa mashtaka yote dhidi yake.

Wakili wa Njenga aitwaye Ndegwa Njiri ndiye alitoa habari hizo leo akitaja hatua hiyo kama ushindi lwa mteja wake. Kulingana naye, DPP ilichukua hatua hiyo kutokana na ukosefu wa ushahidi.

Njenga na wastakiwa wenza 10 walikuwa wanakabiliwa na mashtaka saba yanayojumuisha kuwa wanachama wa kundi haramu la Mungiki na kushiriki vitendo vya uhalifu wa kupangwa katika eneo la Bahati kaunti ya Nakuru.

Uhalifu huo ulidaiwa kutekelezwa kati ya Mei 11 na 18, 2023.

Kesi hii ilianza kwa njia ya kutatanisha Novemba mwaka jana, baada ya mama mkwe wa Njenga ambaye alikuwa shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka kuzirai akila kiapo.

Ushahidi wa kesi hiyo ulitokana na msako uliotekelezwa nyumbani kwa Njenga Mei 12, 2023 na maafisa wa upelelezi wa jinai.

Mmoja wa maafisa hao wa DCI aliambia mahakama kwamba bastola ya mwigo, risasi na bangi ni baadhi ya vitu walivyopata nyumbani kwa Njenga siku hiyo ila yeye hakuwepo.

Walipata pia bastola aina ya Tokarev kwenye kabati ya chumba kikuu cha malazi pamoja na risasi butu tatu. Afisa huyo hata hivyo alikiri mahakamani kwamba Njenga hangetajwa kuwa mmiliki za zana hizo kwa sababu hakuwa mahali zilipatikana.

Share This Article