Mahojiano ya kumtafuta mwenyekiti mpya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Uratibu wa Mipaka IEBC, yameingia siku ya pili leo Jumanne, huku wawaniaji wanne wakitarajiwa kufika mbele ya kamati ya uteuzi.
Miongoni mwa wale watakaofika mbele ya kamati hiyo ni pamoja na Erastus Edung Ethekon, ambaye atahojiwa wa kwanza, akifuatwa na Francis Kakai Kissinger.
Aliyekuwa karani wa bunge ya kaunti ya Nairobi Jacob Ngwele, atakuwa wa tatu kuhojiwa, naye Joy Masinde-Mdivo, ambaye ni mwenyekiti wa bodi ya Kenya Power, akifunga orodha ya watakaohojiwa siku ya Jumanne.
Kamati hiyo ya uteuzi inayoongozwa na mwenyekiti wake Dkt. Nelson Makanda, imejukumiwa kujaza nafasi ya mwenyekiti wa IEBC iliyoachwa wazi na marehemu Wafula Chebukati.
Kamati hiyo imewahakikishia wakenya kwamba itatekeleza mchakato ulio na uwazi, usawa na kwamba wale walio na maadili ya hali ya juu ndio watakaopewa fursa ya kusimamia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.
Mahojiano hayo yanaandaliwa katika chuo cha mafunzo kuhusu huduma ya bima jijini Nairobi, na yanapeperushwa moja kwa moja kupitia runinga ya KBC Channel1.