Katika juhudi za kuhakikisha ufanisi wa mahakama wa ushughulikiaji kesi, Jaji Mkuu Martha Koome amewateua mahakimu 100 watakaoshughulikia kesi za ufisadi na uhalifu wa kiuchumi kote nchini.
“Kuambatana na sehemu ya 3(1) ya sheria dhidi ya ufisadi na uhalkifu wa kiuchuni, Mimi Martha K. Koome Jaji Mkuu na Rais wa Mahakama ya Upeo, nawateua mahakimu wafuatao kushughulikia kesi za ufisadi na uhalifu wa kiuchumi katika vituo vyao vya kazi, na katika vituo ambavyo watahamishiwa,” alisema Koome.
Kupitia kwa gazeti rasmi la serikali la Oktoba 4,2024, Koome alisema mahakimu hao wataendelea kuhudumu katika vituo vyao vya sasa vya mahakama.
Kulingana na Jaji huyo Mkuu, hatua hiyo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kuimarisha uwezo wa mahakama kushughulikia kesi zinazohusiana na rushwa na uhalifu wa kiuchumi, jambo ambalo ni muhimu kwa nchi hii.
Uteuzi huo utakaoanza kutekelezwa kuanzia Jumanne Oktoba 8, unalenga kuongeza ufanisi katika kukabiliana na ufisadi na kuhakikisha uhalifu wa kiuchumi unashughulikiwa kwa wakati ufaao.
Mahakimu hao watafanya kazi katika maeneo mbalimbali, na kuhakikisha kuwa kuna usimamizi kamili wa kisheria ili kushughulikia kesi hizo kwa ufanisi zaidi.
Uteuzi huo umejiri huku kukiwa na wito wa umma wa uwajibikaji, uadilifu na uwazi katika taasisi za serikali.