Mahakama yatupilia mbali mashtaka dhidi ya Imran Khan

Marion Bosire
2 Min Read

Mahakama moja huko Pakistan imetupilia mbali mashtaka yote ya ufisadi dhidi ya aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo Imran Khan.

Mwanasiasa huyo wa umri wa miaka 70 aliwekwa gerezani Agosti 5 baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani kwa kutofichua mali aliyojipatia baada ya kuuza zawadi alizopata akiwa waziri mkuu.

Alikata rufaa na mahakama kuu ya Islamabad ikatupilia mbali mashtaka yote dhidi yake na kuamuru kuachiliwa kwake kwa dhamana.

Naeem Panjutha wakili wa Khan alisema ombi lao kwa mahakama lilikubaliwa na mashtaka pamoja na hukumu vikatupiliwa mbali.

Mwanasiasa wa Pakistan kwa jina Sayed Bukhari alitumia mtandao wa X kutoa maoni yake ambapo alisema kumkamata Khan kwa kesi nyingine kutakuwa na madhara zaidi kwa uadilifu wa kitaifa na sifa ya idara ya mahakama nchini humo.

Jumatatu mahakama kuu ya Balochistan ilitupilia mbali kesi ya uchochezi dhidi ya Khan. Hii ni baada ya maafisa wa mashtaka kukosa kupata idhini hitajika kutoka kwa serikali kuu au serikali ya mkoa ya kuweka kesi dhidi ya Khan.

Mwanzo wa mwezi huu, tume ya uchaguzi nchini Pakistan ilimpiga marufuku Khan kuwania wadhifa wowote kwa muda wa miaka 5 ijayo. Kulingana na sheria za nchi ya Pakistan mtu yeyote ambaye ameshtakiwa hastahili kuongoza chama cha kisiasa, kuwania wadhifa kwenye uchaguzi au kushikilia wadhifa wowote wa uongozi.

Tangu kuondolewa kwake mamlakani Khan ameshikilia kwamba hatua hiyo ilichochewa na Marekani, aliyechukua mahala pake Shehbaz Sharif na jeshi la Pakistan. Wote hao wanakama madai hayo.

Sharif alijiuzulu mwezi huu baada ya muhula wake bungeni kufikia kikomo.

Pakistan inakumbwa na matatizo ya kiuchumi na kisiasa.

Uchaguzi ujao umefanywa kuwa mgumu zaidi baada ya shirika la kutathmini uchaguzi nchini humo kutangaza kwamba lazima uahirishwe kwa muda wa miezi mitatu au minne ili kutoa fursa ya kuundwa upya kwa maeneo bunge kulingana na kura ya maoni ya hivi maajuzi.

Katiba ya Pakistan inaelekeza kwamba uchaguzi uandaliwe Oktoba au Novemba na hadi wakati huo, kaimu waziri mkuu Anwaar-ul-Haq Kakar ataendesha serikali.

Share This Article