Kesi dhidi ya washukiwa 22 waliokamatwa katika bustani ya Mukurwe wa Nyagathanga Disemba 31 mwaka uliopita kwa madai ya kuwa wanachama wa kundi haramu la Mungiki, imeondolewa mahakamani.
Hii ni baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma kuomba kuondoa kesi hiyo.
Kulingana na uamuzi uliotolewa jana Jumatano na Hakimu Mkuu Edwin Nyaga katika mahakama ya Murang’a, kesi hiyo ilitupiliwa mbali chini ya kifungu cha 81(a) cha sheria kuhusu uhalifu.
Hata hivyo, mawakili wa washukiwa hao wakiongozwa na Martha Karua, wameelezea kutoridhishwa kwao na hatua hiyo, wakisema watatumia mbinu zingine za kisheria kuhakikisha wateja wao wanapata haki kutokana na kukiukwa kwa haki zao kuambatana na katiba.
Karua alidokeza kuwa kuondoa kesi hiyo chini ya kifungu 81(a), kunatoa mfano kwamba katika siku zijazo, watu wanaweza tiwa nguvuni na kufikishwa mahakamani kwa madai sawia na hayo.
Washukiwa hao 22 walikamatwa walipokuwa wakishiriki maombi ya kufunga mwaka, na ushaidi uliotolewa dhidi yao ni pombe ya kitamaduni ya Muratina waliopatikana nayo.
“Licha ya kwamba kesi hiyo imeondolewa, jamii ya Wakikuyu itaishi kwa hofu ya kukamatwa inapotekeleza uhuru wa kuabudu,” alisema Karua.
Upande wa mashtaka ulisema Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, iliamua kuondoa kesi hiyo mahakamani ilipobainika kwamba hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuwahukumu washukiwa hao.
“Ushahidi uliotolewa haujabainishwa, na kwa hivyo hatuna lengo la kuendelea kuwashtaki washukiwa,” ulisema upande wa mashtaka.