Mahakama yampata Kimunya na hatia ya unyakuzi wa ardhi

Tom Mathinji
2 Min Read
Aliyekuwa waziri wa Ardhi Amos Kimunya.

Mahakama ya rufaa Jijini Nairobi imemuagiza aliyekuwa waziri wa Ardhi Amos Kimunya kujitetea, katika kesi inayomkabili ya kutoa ardhi ya serikali kwa kampuni moja ya kibinafsi.

Kimunya alishtakiwa pamoja na Lilian Wangiri Njenga ambaye awali alikuwa mkurugenzi wa ugavi wa ardhi na makazi, na Junghae Wainaina Mkurugenzi wa kampuni ya kibinafsi ya Midlands.

Hukumu hiyo iliyotolewa na jopo la majaji watatu, ilithibitisha kuwa ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka, uliwahusisha washtakiwa na kosa hilo na hivyo kutupilia mbali rufaa yao.

Mahakama hiyo ilishikilia umamuzi wa Mahakama Kuu iliyowapata washtakiwa hao na hatia na kuagiza kesi hiyo kurejeshwa kwa Hakimu Mkuu anayeshughulikia kesi za ufisadi na uhalifu wa kiuchumi kwa maelekezo zaidi.

Kimunya na wenzake wameshtakiwa kwa utumzi mbaya wa mamlaka, kukosa kuelezea maslahi ya kibinafsi na uuzaji wa mali ya umma usiozingatia sheria.

Mashtaka yao yalihusisha kukabidhi ardhi ya ekari 25 ya Nyandarua/Njabini/5852, kutoka kwa hazina ya makazi hadi kwa kampuni ya kibinafsi ya Midlands.

Ardhi hiyo awali  ilikuwa  sehemu ya ekari 75, iliyotolewa kwa kituo cha mafunzo ya kilimo cha Njambini, taasisi ya serikali iliyobuniwa kutoa mafunzo kwa wakulima na kupiga jeki maendeleo ya kilimo.

Upande wa mashtaka ulisema washtakiwa hao walifanikisha uhamishaji wa ardhi hiyo hadi kwa kampuni ya Midlands, ambayo Kimunya ni mmoja wa wakurugenzi,bila kufuata taratibu za kisheria zilizopo.

Kesi hiyo awali ilisikizwa na mahakama ya hakimu, ambapo washtakiwa hao walikuwa wamepatikana bila hatia.

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *