Bunge la Seneti liko huru kuendelea mbele na vikao vyake vya kusikiza mashtaka dhidi ya Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Hii ni baada ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Eric Ogola kukataa kuridhia ombi la Gachagua la kuzuia Bunge la Seneti kusikiza mashtaka dhidi yake.
Majaji hao wamesema wamebaini kuwa kesi iliyowasilishwa na Naibu Rais ina msingi na hatadhurika kivyovyote vile ikiwa Seneti itasikiza mashtaka dhidi yake.
“Mshtaki anapaswa kuacha mchakato wa bunge uendelee hadi mwisho wake,” walisema majaji hao katika uamuzi wao leo Jumatano asubuhi.
Waliongeza kuwa watapatiana suluhu juu suala hilo baada ya kukamilika kwa mchakato huo.
Bunge la Seneti limepangiwa kuandaa vikao vya kusikiza mashtaka dhidi ya Gachagua leo Jumatano na kesho Alhamisi.
Mashtaka hayo 11 yaliwasilishwa kupitia hoja maalum ya mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.
Hoja hiyo tayari imepitishwa na Bunge la Taifa.
Mutuse anataka Gachagua kutimuliwa madarakani kwa sababu ya miongoni mwa mambo mengine kueneza ukabila na semi za chuki kinyume cha mahitaji ya wadhifa anaoshikilia.