Mahakama yakataa kusimamisha hoja ya kumbandua Gachagua

Tom Mathinji
1 Min Read
Naibu Rais Rigathi Gachagua

Mahakama Kuu imekataa kutoa maagizo ya kusimamisha mchakato wa bunge la taifa, wa kuandaa hoja ya kumbandua Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Katika uamuzi uliotolea leo Jumatatu, Jaji Bahati Mwamuye alikataa kutoa agizo hilo, kufuatia ombi lililowasilishwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama cha UDA Cleophas Malalah, lililotaka kusitishwa kuwasilishwa na kujadiliwa kwahoja hiyo ya kumbandua Gachagua.

Katika ombi hilo, Malalah alisema kuwa hiyo hiyo inapaswa kusimamishwa, akidokeza kuwa bunge la taifa na lile la Seneti hayajabuniwa kikatiba, kwa kukosa kuafiki hitaji la usawa wa kijinsia kuambatana na katiba.

“Sababu iliyowasilishwa na aliyewasilisha ombi ni kwamba mshtakiwa wa kwanza na wa pili, bunge la taifa na lile la Seneti, hayajabuniwa kikatiba kwa madai kwamba hayajatimiza hitaji la kikatiba la usawa wa kijinsia kuambatana na sehemu ya 27(8) na sehemu ya  81(b) ya katiba ya Kenya.”

Hata hivyo, Jaji Mwamuye alitaja kesi hiyo kuwa ya dharura na kumtaka Malalah kulifahamisha bunge la taifa na lile la Seneti kufikia mwisho wa siku, Septemba 30,2024.

Washtakiwa wamepewa hadi Oktoba 3 kuwasilisha majibu huku kesi hiyo ikipangwa kusikizwa Oktoba 7, 2024.

Share This Article