Mahakama yaharamisha hazina ya ustawishaji maeneo bunge NGCDF

Tom Mathinji
1 Min Read

Mahakama Kuu imetangaza hazina ya serikali ya kitaifa ya ustawi wa maeneo bunge NGCDF iliyobuniwa mwaka 2015, kuwa kinyume cha katiba.

Ikiharamisha hazina hiyo, Mahakama hiyo iliagiza kuwa huduma za hazina hiyo pamoja na miradi yake inayoendelea zitasitishwa Juni 30,2025.

Uamuzi huo, ulitolewa leo Ijumaa na jopo la majaji watatu lililowajumuisha Kanyi Kimondo, Mugure Thande na Roselyn Aburili.

“Tunafahamu kwamba kuna miradi inayotekelezwa na hazina hiyo ya muda mfupi, ile ya wastani na ya muda mrefu. Tuko katikati ya mwaka wa kifedha na fedha tayari zimetegewa miradi inayoendelea,” lilisema jopo hilo la majaji.

Kulingana na Majaji hao, hazina hiyo inahitilafiana na majukumu ya magatuzi na kusababisha kujirudia kwa shughuli au upotevu wa rasilimali adimu.

Mwanaharakati Wanjiru Gikonyo alipinga hazina hiyo mahakamani akiitaja kinyume cha katiba, akidai kuwa inabuni kiwango cha tatu cha usimamizi ambacho hakijanakiliwa na katiba ya nchi hii.

TAGGED:
Share This Article