Mahakama ya Rufaa imeiruhusu serikali kutekeleza Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii, SHIF.
Hata hivyo, majaji Patrick Kiage, Pauline Nyamweya na Ngenye-Macharia wamesitisha utekelezaji wa baadhi ya vipengee vya hazina hiyo hadi kesi iliyowasilishwa mahakamani hapo itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Utekelezaji wa SHIF ulisimamishwa na Mahakama Kuu na kuilazimu Wizara ya Afya kuwasilisha kesi katika Mahakama ya Rufaa kutaka uamuzi huo kubatilishwa.
“Tunaondoa maagizo ya Mahakama Kuu yanayozuia utekelezaji wa sheria ya bima ya afya ya jamii ya mwaka 2023, sheria ya afya ya msingi ya mwaka 2023 na sheria ya afya ya dijitali isipokuwa sehemu zifuatazo za sheria ya bima ya afya ya jamii,” walisema majaji katika uamuzi wao hadi kesi nambari E984 ya mwaka 2023 itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Sehemu za sheria ya bima ya afya ya jamii ya mwaka 2023 ambazo utekelezaji wake umesitishwa na mahakama ni sehemu ya 26(5) inayofanya kuwa lazima kujisajili na kuchangia hazina hiyo kabla ya kupata huduma za umma kutoka kwa serikali kuu na za kaunti au taasisi zao na sehemu ya 27(4) inayoelezea kuwa mtu atapata tu huduma za afya kule ambako michango yao kwa Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii inatolewa.
Utekelezaji wa sehemu ya 47(3) ambayo pia inamtaka kila Mkenya kutambuliwa kwa njia ya pekee ili kupata huduma za afya pia umesitishwa.
SHIF iliratibiwa kuanza kutekelezwa Januari mosi mwaka huu ambapo kila mfanyakazi angetozwa asilimia 2.75 ya mshahara wake kila mwezi ili kuigharimia.
Hazina hiyo inatarajia kuchukua nafasi ya Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya, NHIF ambayo imekuwepo kwa muda mrefu.