Mahakama Kuu: Uteuzi wa makatibu waandamizi 50 ulifanywa kinyume cha sheria

Marion Bosire
2 Min Read

Mahakama Kuu imetangaza kuwa uteuzi wa makatibu waandamizi 50 ulifanywa kinyume cha sheria.

Kwenye uamuzi wa jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo uliotolewa leo Jumatatu, mahakama ilibaini kwamba tume ya utumishi wa umma (PSC) ilikuwa imetenga nafasi 23 kwa ajili ya makatibu waandamizi lakini Rais aliteua 50.

Mnamo mwezi Machi, 2023, mahakama kuu ilizuia makatibu waandamizi 50 ambao walikuwa wameapishwa na Rais kuanza kazi hadi kesi iliyokuwa imewasilishwa na chama cha mawakili nchini, LSK na Katiba Institute isikilizwe na kuamuliwa.

Mahakama hiyo ilizuia pia makatibu hao kupokea mishahara na marupurupu.

Mahakama sasa inatoa ushauri kwa tume ya utumishi wa umma itekeleze uteuzi huo kwa njia inayowiana na katiba ya nchi.

Hata hivyo, mahakama inatambua kwamba katiba haijaweka kiwango cha makatibu waandamizi ambao wanaweza kuteuliwa.

Wakati wa kuunda afisi ya katibu mwandamizi chini ya serikali ya aliyekuwa wakati huo Rais Uhuru Kenyatta, pendekezo lilikuwa kwamba kuwe na katibu mwandamizi mmoja katika kila wizara.

Afisi hiyo iliondolewa na mahakama na kufufuliwa tena kutokana na pendekezo la Rais wa sasa William Ruto.

Ruto aliomba tume ya utumishi wa umma iongeze nafasi za makatibu waandamizi kutoka mmoja katika kila wizara hadi mmoja katika kila idara ya serikali.

Kuhusu suala la kuhususisha umma katika uteuzi wa makatibu waandamizi, ambalo ni hitaji la kikatiba, mahakama iliamua kwamba hata ingawa umma ulihusishwa, maoni ya umma hayakugusia nafasi 27 zaidi ambazo ziliongezwa.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *