Mahakama Kuu yaruhusu KDF kushika doria

Tom Mathinji
2 Min Read
Maafisa wa vikosi vya ulinzi KDF washika doria katikati mwa Jiji la Nairobi.

Jaji wa Mahakama Kuu High Lawrence Mugambi amesema serikali haikuvunja sheria kuwatuma maafisa wa vikosi vya ulinzi KDF, kushika doria kuwasaidia maafisa wa polisi kukabiliana na waandamanaji.

Katika kesi iliyowasilishwa na chama cha wanasheria nchini LSK, dhidi ya afisi ya Mwanasheria Mkuu na waziri wa ulinzi, Jaji Mugambi aliamua kuwa vikosi vya KDF vitaendelea kushika doria kwa ushirikiano na maafisa wa polisi kwa siku mbili zaidi, wakati ambapo atatoa maelekezo zaidi.

Alisema hadi wakati huo, wanajeshi hao watawasaidia maafisa wa polisi kudumisha sheria na amani.

Hata hivyo Jaji huyo aliitaka serikali kuelezea wanajeshi watashika doria kwa muda gani, maeneo yanayolengwa katika doria hizo na kwanini kikosi cha KDF kitumiwe kushika doria.

Mnamo siku ya Jumatano, bunge lilipitisha kupelekwa kwa vikosi vya ulinzi nchini KDF, kuwasaidia maafisa wa polisi kukabiliana na waandamanaji waliokuwa wakipinga Mswada wa Fedha wa mwaka 2024.

Siku ya Alhamisi, wanajeshi walionekana wakiingia katika eneo la katikati ya jiji la Nairobi na barabara kuu za kuingia na kuondoka jijini, kwa magari yao ya kivita na zana za kijeshi.

Aidha maafisa hao wa kijeshi walishika doria katika majengo muhimu ya serikali, na katika sehemu mbali mbali za Jiji kuu Nairobi.

Hata baada ya Rais William Ruto kutangaza hatatia saini mswada huo kuwa sheria, waandamanaji bado walikabiliana na maafisa wa usalama jijini Nairobi Alhamisi.

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *