Mahakama Kuu imebatilisha uamuzi wa kubadilisha jina la barabara ya Dik Dik mtaani Kileleshwa katika kaunti ya Nairobi hadi jina la Francis Atwoli.
Serikali ya kaunti ya Nairobi ilifanya mabadiliko hayo Mei 28, 2021 kama njia ya kumuenzi mtetezi huyo wa wafanyakazi.
Francis Atwoli ndiye Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini, COTU.
Hata hivyo, mzozo ulizuka katika eneo la Dik Dik baada ya watu wasiojulikana kung’oa mlingoti uliokuwa na jina hilo jipya la barabara ya Dik Dik na kuuchoma.
Serikali ya kaunti ilisimika tena mlingoti huo na kuweka kamera za ulinzi kuhakikisha hauharibiwi tena.
Baadaye, baadhi ya wakazi wa eneo la Dik Dik walikwenda mahakamani kupinga hatua ya kubadilisha jina la barabara hiyo.
Katika uamuzi wake hivi leo, Mahakama Kuu ilisema wananchi hawakuhusishwa katika mchakato mzima wa kubadilisha jina la barabara hiyo inavyohitajika kisheria.