Mahakama kuhudumu Jumatano licha ya tishio la LSK

Chama cha LSK kimetoa wito kwa wanachama wake nchini kote kususia kesi mahakamani Julai 22 kulalamikia ufisadi na utovu wa maadili.

Martin Mwanje
2 Min Read
Jaji Mkuu Martha Koome

Idara ya Mahakama imesema mahakama nchini kote zitahudumu kama kawaida keshokutwa, Jumatano, Julai 22. 

Hii ni licha ya wanasheria nchini kupitia kwa chama chao cha LSK kutangaza mpango wa kususia huduma za mahakama kupinga kile kinachokitaja kuwa kukithiri kwa ufisadi na utovu wa maadili katika idara hiyo.

“Idara ya Mahakama haizingatii kususia kesi mahakamani kuwa mwitikio mwafaka au wenye uwiano kwa masuala yaliyoibuliwa. Hatua kama hiyo itawaathiri maafisa wa mahakama na watumiaji wengine ambao kesi zao zimepangwa kusikilizwa na kuamuliwa,” ilisema idara hiyo kupitia kwa msemaji wake Paul Ndemo kwenye taarifa.

“Idara ya Mahakama inaahikishia umma kuwa mahakama zote katika nchini kote zitafunguliwa na zitaendelea kusikiliza na kuamua kesi kama ilivyopangwa Jumatano, Julai 22,  2026.”

Idara hiyo sasa inatoa wito kwa wanasheria nchini kuwa tayari kufanya mazungumzo ili kuangazia malalamishi yoyote ambayo yanawakuna kichwa kuhusiana na utendaji kazi wa idara hiyo.

LSK imewshutumu baadhi ya maafisa wa mahakama kwa matumizi mabaya ya mamlaka, mienendo isiyo ya kimaadili, na vitendo ambavyo vimedhoofisha imani ya umma katika mfumo wa utoaji haki nchini.

Kimetaja pia kucheleweshwa kwa usimamizi wa kesi, uzembe katika sajili za mahakama na hitilafu za mara kwa mara katika mifumo ya uwasilishaji wa nyaraka kwa njia ya kielektroniki kama mambo yanayodhalilisha hadhi ya taaluma ya uanasheria.

Akizungumza mjini Machakos mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais wa LSK Charles Kanjama alisema mpango wa kususia mahakama kwa siku moja utawazuia wanachama wake kushiriki kusikilizwa kwa kesi na maombi mahakamani.

Kanjama alifafanua kuwa uwasilishaji wa kesi mpya utaendelea kama kawaida, huku kutajwa kwa kesi na maombi yanayohusu maagizo ya muda kukiendelea tu kwa madhumuni ya kupata tarehe mpya za kusikilizwa au kuongeza muda wa maagizo hayo.

Share This Article