Magunia milioni 61 ya mahindi kuvunwa mwaka huu, asema Rais Ruto.

Martin Mwanje
1 Min Read

Idadi ya mahindi yanayotarajiwa kuvunwa mwaka huu kote nchini ni magunia milioni 61. 

Hili litakuwa ongezeko la magunia milioni 17 ikilinganishwa na magunia milioni 44 yaliyovunwa mwaka jana.

Wakulima aidha walipanda ekari laki mbili mpya za mahindi mwaka huu.

Rais William Ruto amehusisha mavuno mengi yanayotarajiwa na hatua iliyochukuliwa na serikali ya Kenya Kwanza mapema mwaka huu kupunguza bei ya mboolea kutoka shilingi elfu 7 hadi 3,500.

“Mwaka uuliopita, tulivuna magunia milioni 44 kwa sababu wakulima hawakuweza kugharimia bei ya mbolea ambayo ilikuwa juu sana. Lakini mwaka huu, kwa sababu tumeweka mpango mzuri, tumepunguza gharama ya mbolea, mavuno ambayo tunatarajia ambayo yameanza kuja ni magunia milioni 61,” alisema Rais Ruto wakati akitoa hotuba katika kanisa la ACK alikoweka jiwe la msingi la ujenzi wa kanisa hilo, kaunti ya Kiambu leo Alhamisi.

“Wakulima milioni tano walisajiliwa mapema mwaka huu.  Lakini wengine hatukuwapata. Tunataka kusajili wakulima zaidi ndio tuwe na rejesta ili watusaidie kuzalisha chakula, tundoe njaa na tuweke pesa katika mifuko yetu tufukuze umaskini.”

Serikali imetangaza kupunguzwa zaidi kwa bei ya mbolea kutoka shilingi 3,500 hadi 2,500 katika juhudi za kuongeza uzalishaji wa chakula nchini.

 

 

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *