Magavana watakiwa kuondoa kesi ya kunyimwa fedha za hazina ya barabara

Marion Bosire
2 Min Read
Ndindi Nyoro, mwenyekiti wa kamati ya bajeti bungeni

Bunge la taifa linawataka magavana kuondoa kesi waliyowasilisha mahakamani kupinga hatua ya bunge ya kuwanyima shilingi bilioni 10.5 kutoka kwa hazina ya barabara.

Wanachama wa kamati ya bunge la taifa kuhusu upatanishi jana waliwataka maseneta kuingilia kati ili kuhakikisha magavana wanaondoa kesi hiyo mahakamani.

Kulingana nao, hatua hiyo itaamua jinsi mazungumzo kuhusu mgogoro wa mgao wa fedha kwa kaunti yataendelea.

Upatanishi huo ulijiri baada ya maseneta kufanyia marekebisho mswada wa ugavi wa mapato wa mwaka 2024, na kutoa shilingi bilioni 400 kwa magatuzi badala ya bilioni 380 zilizopendekezwa na bunge la taifa.

Wito uliotolewa katika kikao cha pamoja chini ya uenyekiti wa Ndindi Nyoro mwenyekiti wa kamati ya bajeti ya bunge na Ali Roba mwenyekiti wa kamati sawia katika seneti ni kwamba mazungumzo yatarahisishwa iwapo kesi hiyo itaondolewa.

Mahakama kuu iliongeza muda wa agizo la kufunga ugavi wa fedha kutoka kwa hazina ya barabara kusubiri kuamuliwa kwa kesi iliyowasilishwa na baraza la magavana.

Wakiongozwa na mbunge wa Funyula Wilberforce Oundo, wabunge wa bunge la taifa wanahisi kwamba mgogoro wa mswada wa ugavi wa mapato umechochewa na siasa.

Lakini Roba alisema maseneta wanatekeleza jukumu lao la kulinda magatuzi katika kushinikiza mapato zaidi kwa kaunti na wala wao sio vibaraka wa magavana.

Wabunge walisisitiza hakuna muda wa kuharibu ili kujumuisha bilioni 20 zaidi wanazosaka magavana.

Nyoro aliwataka wanachama wa kamati ya bajeti kutafuta suluhu la kimakusudi na kwamba sio lazima watumie njia rahisi.

Alipendekeza kwamba ikiwezekana bunge la seneti linafaa kuandaa mazungumzo na baraza la magavana ili kuhakikisha wanahudhuria majadiliano kuhusu suluhisho.

Share This Article