Magavana wa kaunti zote 47 wametakiwa kuhakikisha wanaweka dawa na vifaa vya kutosha katika hospitali mbalimbali za umma zilizopo katika kaunti zao.
Aidha, Rais William Ruto amewataka Magavana hao kuhakikisha wanawaajiri wahudumu wa afya wa kutosha ili kusaidia kufanikisha juhudi za serikali za upatikanaji afya kwa wote.
Akizungumza leo Jumatatu wakati za ziara ya kuzindua mradi wa umeme wa Paranga katika eneo la Wundanyi, kaunti ya Taita Taveta, Rais Ruto alisisitiza umuhimu wa serikali kuu kushirikiana na serikali za kaunti ili kuhakikisha ajenda ya utoaji huduma bora za afya kwa raia inafanikiwa.
Wakati huohuo, Ruto aliendelea kueneza injili ya kuwataka Wakenya kujisajili na Mamlaka ya Afya ya Jamii ya SHA ili kuhakikisha wanapata huduma bora za matibabu.
“Kama wewe hujajiandikisha, sasa utaisaidika namna gani? Na usingoje hadi uwe mgonjwa ndio ujisajili. Kujiandikisha ni bure,” Ruto aliwasihi wakazi wa eneo hilo akiwa ameandamana na Gavana wa kaunti ya Taita Taveta Andrew Mwadime.
Rais Ruto ameelezea imani kuwa licha ya SHA kukumbwa na changamoto katika hatua za kwanza za utekelezaji wake, mpango huo utahakikishia kuwa kila Mkenya anapata huduma bora za afya bila kujali hadhi yake katika jamii.