Baraza la Magavana (CoG) limekuja kwa matao ya juu na kukanusha kwa kinywa kipana, taarifa zilizochapishwa na Mdhibiti wa Bajeti kuashiria kuwa kaunti kumi hazikutumia hela walizotengewa katika robo ya kwanza ya mwaka huu.
Mwenyekiti wa CoG Ahmed Abdullahi amesema kuwa kaunti hazingetumia hela hizo kwani zilikuwa hazijatolewa na hazina kuu.
Mdhibiti wa Bajeti Dkt. Margaret Nyakang’o kwenye ripoti yake alisema kuwa kaunti 10 hazikutumia hata senti moja walizotengewa katika miezi ya Julai, Agosti na Septemba.
Abdullahi ameitaja ripoti hiyo kuwa yenye nia mbovu na iliyolenga kuchafua sifa za Magavana, wakati ambapo serikali kuu ilichelewesha utoaji wa pesa hizo.
Kaunti zilizomulikwa katika ripoti hiyo ni:- Nairobi, Baringo, Elgeyo Marakwet, Kajiado, Kisii,Lamu, Uasin Gishu, Nyandarua, Tana River na West Pokot.