Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha katika Baraza la Magavana nchini, ambaye pia ni Gavana wa Kakamega, Fernandes Barasa, ametamaushwa na mchakato unaoendelea kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha kwa serikali za magatuzi, akieleza kuwa umesababisha kaunti kusalia katika hali ya siutofahamu.
Akizungumza katika Bunge la Kakamega wakati wa kutoa hotuba ya serikali yake, Barasa amelihimiza Bunge la Taifa kuondoa vikwazo vinavyokwamisha mswada wa kuongeza mgao wa fedha kwa serikali za kaunti.
Pia amelitaka bunge hilo kuachilia shilingi bilioni 10.5 ili kuwezesha magatuzi kufanikisha miradi yao kikamilifu.
Gavana huyo amesema anashirikiana na serikali ya taifa katika kukamilisha miradi ya kaunti, ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Kakamega Level 6 na uwanja wa Bukhungu.
Amewahimiza wawakilishi wa wadi kushirikiana ili kuhakikisha miradi ya kaunti inakamilika kwa wakati unaofaa.
Vilevile, Barasa amewahimiza wakazi wa Kakamega kujisajili kwa wingi katika bima ya afya ya SHA ili kuepuka changamoto za kifedha pale wanapopata matatizo ya kiafya.