Maafisa wa kliniki wamesitisha mgomo wao ulioanza katikati ya mwezi jana kulalamikia hatua ya serikali kushindwa kutekeleza makubaliano yao ya awali ya kurejea kazini.
Aidha, maafisa hao walilalamikia kutengwa katika kuwahudumia wagonjwa chini ya mfumo mpya wa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA).
Waziri wa Afya Dkt. Deborah Barasa amesema maafisa wa kliniki walikubali kusitisha mgomo wao baada ya kutia saini Mkataba wa Maelewano na Wizara ya Afya na Baraza la Magavana.
Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo ilifanyika leo Jumatano katika makao makuu ya Wizara ya Afya jijini Nairobi na maafisa wa kliniki kutakiwa kurejea kazini ndani ya saa 24 zijazo.
“Leo, ningependa kutangaza kuwa kufuatia mazungumzo yenye tija, mgomo wa maafisa wa kliniki umefutiliwa mbali kufuatia mazungumzo kati ya Wizara ya Afya na uongozi wa chama cha maafisa wa kliniki,” alisema Dkt. Barasa kwenye taarifa.
“Hii ni hatua muhimu katika kuimarisha mfumo wetu wa afya kupitia mazungumzo na maelewano ya pande mbili.”
Waziri Barasa ameahidi kuwa serikali imedhamiria kuangazia masuala yote yaliyoibuliwa na maafisa wa kliniki wakati pia ikihakikisha mahitaji ya Wakenya wote yanatimizwa bila usumbufu wowote.
“Kwa hivyo, nawashukuru maafisa wote wa kliniki ambao kwa hiari yao wenyewe wameazimia kurejea kazini mara moja na kuwasihi kuendelea kufanya kazi kuelekea kujenga mfumo thabiti wa afya wenye kuwajali mno wagonjwa ambao unatoa hakikisho la huduma za gharama nafuu za matibabu kwa Wakenya wote.”
Kumekuwa na migomo ya mara kwa mara ya wahudumu wa afya nchini wanaolalamikia mazingira mabovu ya utendakazi, kukosa kupandishwa vyeo na kuongezwa mshahara, matakwa ambayo wanaishinikiza serikali kuangazia ili kuboresha mazingira ya utendakazi.