Irene Mayaka achaguliwa mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu utangamano wa kikanda

Mbunge wa eneo la Fafi, Farah Salah naye alichaguliwa kuwa naibu mwenyekiti wa kamati hiyo.

Marion Bosire
2 Min Read

Mbunge mteule wa chama cha ODM Irene Mayaka amechaguliwa bila kupingwa kama mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu utangamano wa kikanda.

Wadhifa wa naibu mwenyekiti wa kamati hiyo, umechukuliwa na mbunge wa eneo la Fafi, Farah Salah, ambaye pia alichaguliwa bila upinzani kufuatia uamuzi wa Makali Mulu kujiondoa kwenye kinyang’anyiro.

“Nimejiondoa kwa ajili ya Mheshimiwa Farah ili aendelee kuwa Naibu Mwenyekiti. Nitaendelea kuwa mwaminifu kwa Wakenya na kutimiza wajibu wangu kama mwanachama wa kamati hii,” alisema Mulu.

Wanachama wa Kamati walitambua kazi nzuri aliyofanya mwenyekiti anayeondoka Wanjiku Muhia ambaye ni mbunge wa Kipipiri na kuahidi kuunga mkono uongozi mpya wa kamati hiyo.

Huku akidhihirisha kwamba anaunga mkono uongozi mpya, mbunge wa Kipipiri aligusia baadhi ya mafanikio yaliyopatikana hadi sasa na kamati kama kuboresha idara ya uhamiaji iliyopunguza muda wa kutengeneza pasi ya kusafiri hadi siku 7.

Kwa upande wake, Mbunge wa Fafi alimshukuru Mulu kwa kujiondoa na kutaka wanachama wa kamati hiyo kuendelea na ushirikiano waliodhihirisha awali.

“Hatukuwahi kukosa akidi katika kamati hii. Tuendelee kwa moyo huo huo,” alisema Farah.

Akihutubia kamati baada ya uchaguzi, Mayaka alishukuru wanachama kwa kumuunga mkono na kuhimiza ushirikiano na uthabiti katika kuhudhuria vikao vya kamati.

“Kwa msaada wenu, mimi na naibu mwenyekiti tutaipeleka kamati hii katika kiwango cha juu zaidi,” aliahidi Mayaka.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *