Magavana: Tunahitaji shilingi bilioni 15 kukabiliana na athari za El Nino

Martin Mwanje
1 Min Read

Kaunti zinahitaji jumla ya shilingi bilioni 15 ili kuepusha, kupunguza na kukabiliana na athari za mvua ya El Nino.

Kati ya shilingi hizo, Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Anne Waiguru anasema kaunti zina shilingi bilioni 1.9 pekee za kukabiliana na athari hizo, ikiashiria kuna nakisi ya shilingi bilioni 13.

“Hii ina maana kwamba serikali kuu na washirika wa kimaendeleo wanahitaji kusaidia kugharimia nakisi hiyo,” alisema Waiguru katika taarifa leo Jumatatu.

“Kwa sasa, kaunti 35 zimewasilisha mipango yao ya maandalizi ya mvua ya El Nino, ambayo imekabidhiwa Ofisi ya Naibu wa Rais.”

Waiguru anasema wakati wa ukame wa muda mrefu ulioshuhudiwa nchini miezi michache iliyopita, shughuli hazikuratibiwa vizuri na mwitikio wa serikali kuu ulikawia.

Kwa misingi hiyo, Baraza la Magavana linasema mwitikio wowote utolewe kupitia kwa Ofisi ya Baraza la Magavana na kwamba ufadhili kwa nakisi inayohitajika utolewe kwa kaunti.

“Hii itahakikisha jitahada za kukabiliana na athari ya mvua ya El Nino zinaratibiwa vizuri ili kuepusha urudufu na utumiaji mbaya wa rasilimali,” aliongeza Waiguru.

 

 

Share This Article