Mahakama kuu imeamua leo kwamba magavana na manaibu gavana wanaostaafu hawatapokea malipo ya baada ya kustaafu kama ilivyo kwa maafisa wakuu katika serikali ya kitaifa.
Uamuzi huu umetolewa na jaji Lawrence Mugambi leo Jumatano Julai 31, 2024 katika mahakama kuu ya Nairobi na unafuatia kesi iliyowasilishwa mahakamani na baraza la magavana nchini COG dhidi ya tume ya mishahara na marupurupu nchini SRC.
Katika taarifa iliyotolewa baada ya uamuzi huo, SRC imeelezea kwamba mpango uliopendekezwa wa kuwapa magavana na manaibu gavana wastaafu malipo hauwezi kuafikiwa nchini.
Iwapo ungetekelezwa basi mpango huo ungesababisha athari kwa maafisa wote wa serikali kuu na serikali za kaunti na kusababisha serikali kutumia pesa nyingi huko, huku maendeleo yakitengewa raslimali kidogo.
SRC inasema pia kwamba mpango huo ungekuwa mzigo mkubwa kwa magavana wanaofuata pamoja na umma kwa jumla kwani ushuru wao ungetumika kulipa marupurupu kwa muda mrefu sana.
Tume hiyo imebainisha kwamba tayari viongozi hao wanapatiwa takrima na ainatosha kuwalinda baada ya kustaafu.
“Hata ingawa magavana na manaibu gavana ni maafisa wa serikali, sio maafisa wote wa serikali wametengewa mpango wa malipo baada ya kustaafu.” SRC ilielezea kwenye taarifa.