Magava wanawake wasema Kenya iko tayari kwa naibu Rais mwanamke

Tom Mathinji
2 Min Read
Magavana wanawake washinikiza wanawake wapate nafasi zaidi za uongozi.

Magavana wanawake wamesema kuwa Kenya iko tayari kwa naibu Rais mwanamke huku wakimtaka mwenzao wa Kirinyaga Ann Waiguru kuwania wadhifa huo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.

Magavana hao walisema Waiguru amethibitisha ana uwezo wa kushikilia wadhifa wa naibu wa Rais.

Wakizungumza katika kaunti ya Machakos wakati wa mkutano uliowaleta pamoja Magavana wanawake hapa nchini, viongozi hao walisema Waiguru  ameonyesha ujuzi wa hali ya juu akiwa mwenyekiti wa Baraza la Magavana nchini.

Matamshi ya Magavana hao yaliungwa mkono na aliyekuwa Gavana wa Kitui Charity ngilu, aliyemhimiza Waiguru kutolegeza kamba katika kutafuta wadhifa huo wa juu, ikiwa ni pamoja na ile ya Rais.

Ngilu alisema ikizingatiwa kuwa Waiguru alihudumu wadhifa wa waziri na sasa anahudumu muhula wa pili akiwa Gavana, ameonyesha anastahili sasa kutwaa wadhifa wa juu.

“Hakuna aliye na tajiriba kubwa kukushinda. Umekuwa waziri na sasa wewe ni Gavana kipindi cha muhula wa pili, kwa hivyo hupaswi kuogopa kusonga mbele,” alisema Ngilu.

Kwa upande wake Gavana wa Kwale Fatuma Achani, alisema Gavana Waiguru ameongoza Baraza la magavana kwa ustadi wa kupigiwa mfano, na amehitimu kwa wadhifa wa naibu wa Rais.

“Mwenyekiti wetu ametuongoza vyema, umepeleka baraza hilo katika kiwango cha juu na kuna utulivu. Umehitimu kwa wadhifa wa juu,” alisema Achani.

Alipozungumza, Waiguru alitoa wito kwa Wakenya kuunga mkono wanawake wengi kuchukua nyadhifa za uongozi ili kupiga hatua katika kutimiza usawa wa kijinsia.

Alisema Magavana wanawake ambao wanakamilisha muhula wao wa pili, wanapaswa kupewa fursa ya kuhudumia taifa hili katika nyadhifa za juu.

Alidokeza kuwa mkutano huo wa Magavana wanawake almaarufu G7, unalenga kuongeza idadi ya Magavana wanawake kutoka 7 hadi 24 katika uchaguzi ujao mwaka 2027.

Magavana wao walijumuisha Fatuma Achani (Kwale), Gladys Wanga (Homa Bay), Cecil Mbarire (Embu), Wavinya Ndeti (Machakos) Susan Kihika (Nakuru).

Website |  + posts
Share This Article