Magaidi watatu waliojihami kwa silaha waliuawa mjini Kisii jana usiku na bunduki aina ya AK 47 kupatikana.
Hii ni baada ya magaidi hao kujaribu kuwakwepa maafisa wa polisi waliokuwa wakiwasaka kutoka Migori hadi Kisii.
Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI inasema magaidi hao walikuwa wamepanga kutekeleza shambulizi mjini Kisii.
Baada ya kupata tetesi za kuwepo kwa kundi hilo la magaidi, wapelelezi wa DCI walitathmini namna kundi hilo linavyoendesha shughuli zake kwa kuzingatia wizi wa mabavu wa awali uliofanywa na kundi hilo kabla ya kuanzisha msako dhidi yake.
Wakijihami kwa bunduki aina ya AK 47 na silaha zingine, magaidi hao waliabiri pikipiki wakiwa tayari kwenda mawindoni.
“Lakini mipango yao ilitibuliwa na timu ya wapelelezi waliowafuata magaidi hao watatu kwa umbali wa zaidi ya kilomita 60 kabla ya kuwakamata katika eneo la Corner Mbaya mjini Kisii,” inasema DCI katika taarifa.
“Magaidi hao waliuawa na makachero baada ya kukaidi agizo la kuwataka kujisalimisha.”
DCI inasema bunduki aina ya AK47 iliyokuwa na risasi 21, silaha aina ya Rambo, panga na pikipiki yenye nambari ya usajili KMGH 656X vilipatikana wakati wa msako huo.
Moja wa washukiwa alitambuliwa kama Joseph Mwita mwenye umri wa miaka 27 kutoka eneo la Kuria kaunti ya Migori, huku wengine wawili wanaokisiwa kuwa na umri wa miaka 30 wakisubiri kutambuliwa katika hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii.
DCI imeahidi kukabiliana vikali na magaidi wanaowahangaisha raia nchini.