Mafuriko ya muda yasababisha vifo Indonesia

Marion Bosire
2 Min Read

Mafuriko ya muda na maporomoko ya ardhi katika kisiwa cha Sumatra nchini Indonesia vimesababisha vifo vya watu wapatao 19 huku wengine saba wasijulikane waliko kulingana na maafisa katika eneo hilo.

Tope, mawe pamoja na miti iliyong’oka viliangushwa kutoka kilimani na kufunika vijiji vya wilaya ya ya Pesisir Selatan mkoa wa Sumatra Magharibi Ijumaa jioni kufuatia mvua kubwa.

Haya ni kulingana na Doni Yusrizal, ambaye anaongoza afisi ya kusughulikia majanga katika eneo husika.

Alisema wanaotekeleza shughuli za uokoaji walipata miili 7 katika kijiji cha Koto XI Tarusanna na mingine mitatu katika vijiji viwili vilivyo karibu.

Shughuli za uokoaji hata hivyo zilitatizwa na kukatika kwa umeme na barabara ambazo hazipitiki zilizojaa tope na uchafu wa aina nyingine.

Shirika la kitaifa la kushughulikia majanga nchini Indonesia lilitangaza kupatikana kwa miili 6 huko Pesisir Selatan na mitatu katika wilaya jirani ya Padang Pariaman, na kufikisha idadi ya vifo kuwa 19.

Watu wawili walithibitishwa kupata majeraha kwenye tukio hilo, saba hawajulikani waliko na zaidi ya elfu 80, wametorokea makazi ya muda waliyopatiwa na serikali.

Mafuriko ya muda mfupi na maporomoko ya ardhi ni jambo la kawaida nchini Indonesia, ambapo watu wengi wanaishi katika maeneo yaliyo katika hatari ya kukumbwa na mafuriko hasa msimu wa mvua kubwa.

Disemba mwaka jana watu wawili walifariki wakati wa tukio sawia lililoharibu makazi ya watu kadhaa na hoteli moja karibu na Ziwa Toba huko Sumatra.

Share This Article