Mafundi wa Jua kali Kibera wapokea malipo kwenye sherehe za mashujaa

Marion Bosire
2 Min Read
Charles Hinga, Katibu wa Nyumba

Ikikumbukwa kwamba mada ya sherehe za mwaka huu za mashujaa ni nyumba za bei nafuu nchini, mafundi wa Jua Kali katika eneo la Kibera kaunti ya Nairobi walilipwa kwenye sherehe hizo.

Mkandarasi wa mradi wa nyumba za bei nafuu wa Kibera Soweto pamoja na mwenyekiti wa chama cha mafundi wa Jua kali wa Kibera walikabidhiwa hundi ya shilingi milioni 720 na Rais William Ruto.

Mafundi hao wanatekeleza jukumu muhimu katika ujenzi huo ambapo wanatengeneza milango, madirisha na fremu za nyumba za mradi huo wa nyumba za bei nafuu.

Katibu wa nyumba Charles Hinga aliongoza hafla hiyo ambapo pia alimwita mmoja wa watakaonufaika na malipo hayo na hatimaye nyumba hizo zitakapokamilika.

Stanley mkazi wa eneo la Soweto huko Kibera alishukuru Rais Ruto kwa malipo akisema kazi wanayofanya kwenye mradi huo wa nyumba za bei nafuu ndiyo inaendesha uchumi wa eneo wanaloishi.

Kijana huyo alidhihirisha imani ya makazi bora siku za usoni akiamini kwamba atakuwa mmoja wa watakaonufaika. Alitoa taswira ya makazi mabovu wanayoishi kwa sasa huku akishukuru sana kwa mradi huo.

Katibu Hinga alifichua pia kwamba Kenya imetambuliwa katika bara Afrika kutokana na mradi wa nyumba za bei nafuu unaolenga kuboresha makazi ya watu.

Aliwatambulisha pia viongozi wa wanafunzi wa vyuo mbali mbali nchini ambao alisema wameidhinisha miundo ya makazi ya wanafunzi ambayo yataanza kujengwa hivi karibuni.

Share This Article