Maeneo kame yabashiriwa kuathirika na mafuriko

Marion Bosire
2 Min Read

Kaunti ambazo ziko kwenye maeneo kame nchini huenda zikaathiriwa na mafuriko wakati wa mvua inayotarajiwa ya El Nino.

Waziri wa Jumuiya ya Afrika mashariki, Maeneo Kame na Maendeleo ya Kikanda Rebecca Miano kwenye taarifa alitaja kaunti za Marsabit, Turkana, Baringo, Samburu, Wajir, Garissa, Tana River, Kilifi, Kwale, Taita Taveta, Mandera, Narok na Isiolo kuwa zilizo kwenye hatari kubwa ya kukumbwa na mafuriko.

Alisema kaunti za Elgeyo Marakwet na Pokot Magharibi huenda zikakumbwa na maporomoko ya ardhi.

Waziri Miano alisema kwamba kuanzia mwezi Agosti, mamlaka ya kushughulikia ukame ambayo iko chini ya wizara yake imekuwa ikiandaa mikutano na kaunti zote za maeneo kame kujiandaa kwa mvua hiyo kubwa ya El Nino.

Mikutano hiyo iliangazia uhamasishaji, uundaji wa kamati za kiufundi za kushughulikia hali, utambuzi wa maeneo ambayo huenda yakaathirika, maandalizi ya bajeti ya kugharimia madhara ya mvua hiyo na kuanzishwa kwa makundi ya mtandao wa Whatsapp kati ya masuala mengine.

Viongozi husika wameelekezwa wahamasishe jamii za maeneo yao kuhusu mvua hiyo kabla haijaanza na ikianza wawe waangalizi wa nyanjani na kutoa taarifa ipasayo.

Baada ya mvua hiyo, watahitajika kutathmini madhara na kuanzisha mipango ya kurejesha hali ya kawaida.

Utabiri wa hali ya hewa unaashiria kwamba mvua hiyo kubwa ya El Nino inatarajiwa kati ya mwezi huu wa Oktoba hadi Disemba.

Share This Article