Maclean asema alitiliwa dawa kwenye sharubati

Marion Bosire
1 Min Read

Godfrey Mwaijonga MacLean ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya habari mitandaoni nchini Tanzania iitwayo Dar 24 Media aliyetoweka Oktoba 31, 2024 amepatikana.

Maclean alipatikana katika eneo la Buyuni wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Alipatikana usiku wa Novemba 2, 2024 na alielezea kwamba hakutekwa nyara nje ya afisi yake walivyofikiria wengi, bali alikwenda mwenyewe hadi Kigamboni.

Dhamira ilikuwa kufanya mkutano na wanabiashara wenza ambao anasema walimtilia sumu kwenye kinywaji cha sharubati akapoteza fahamu.

Anasema alipozinduka, watu hao walimshikiniza awape nywila za akaunti za benki anazosimamia na za mitandao ya kijamii.

Mwaijonga baadaye alitiwa kwenye gari na kuzungushwa kwa muda mrefu na watu hao walipoona kwamba amekataa kuwapa walichokata, wakambwaga Buyuni.

Alikuwa akizungumza katika kituo cha polisi cha Central jijini Dar es Salaam jana usiku akiwa na Kamanda wa polisi wa Kanda ya Dar es salaam aitwaye Jumanne Muliro na watu wa familia yake.

Muliro anasema alipokea taarifa za kupatikana kwa Maclean kupitia kutoka kwa baba mzazi ambaye pia alifahamishwa kupitia mawasiliano ya simu na msamaria mwema aliyempata.

Kamanda huyo aliandamana na wanafamilia hadi Buyuni ambako walimpata Maclean na kumpeleka hospitali kwa vipimo akapatikana kuwa sawa.

Share This Article