Mhubiri tata Paul Makenzi, mkewe Rhoda Maweu na washukiwa wengine 93 leo walifikishwa mahakamani huko Mombasa ambako wameshtakiwa kwa visa 238 vya kuua bila kukusudia.
Washukiwa hao ambao wamekuwa rumande katika gereza la Shimo la Tewa kwa karibu miezi 9 walikana mashtaka yote dhidi yao.
Washukiwa 35 kati ya hao 95 wanatarajiwa kufikishwa kwenye mahakama ya watoto ya Tononoka Alhamisi kwa makosa ya kushambulia na kudhulumu watoto pamoja na kukiuka haki yao ya kupata elimu.
Vifo vya wafuasi wa Mackenzie katika msitu wa Shakahola vinaaminika kutokea kati ya mwaka 2019 na 2023 na kufikia sasa miili karibu 400 imefukuliwa kutoka eneo hilo.
Mackenzie anasemekana kutoa mafundisho yenye itikadi kali kwa wafuasi wake ambao walifunga kula na kunywa hadi kufa.
Yeye na washukiwa wenza wamefikishwa mahakamani baada ya afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma kubainisha kwamba ushahidi uliokusanywa unatosha kuwafungulia mashtaka.