Mackenzie asusia kikao cha mahakama

Marion Bosire
2 Min Read

Mshukiwa mkuu wa mauaji ya Shakahola Paul Nthenge Mackenzie amesusia kikao cha mahakama kuhusiana na kesi inayomkabili na wenzake 94.

Kesi hiyo ya mauaji ambayo ilitarajiwa kusikilizwa leo Jumatano ilikuwa inahusiana na ombi la upande wa mashtaka kupinga kuachiliwa kwa Mackenzie na washukiwa wengine kwa dhamana.

Wakili wa Mackenzie Wycliffe Makasembo alijaribu kumshawishi mhubiri huyo mwenye utata kuhudhuria kikao hicho ila akakataa. Hakuenda popote ila alisalia katika maeneo ya mahakama hiyo ya Shanzu.

Makasembo aliambia Hakimu Mwandamizi Leah Juma kuwa mteja wake alilalamikia kutengwa kwake na wenzake na kusema kuwa huo ulikuwa ubaguzi.

Wakili huyo wa Mackenzie alifahamisha mahakama kuwa mteja wake alihofia ‘kutekwa nyara’.

Aliomba mahakama kuhairisha kesi hiyo ili amfahamishe Mackenzie kuhusu masuala ya sheria na kumshawishi ahudhurie vikao vya mahakama.

Msaidizi Mwandamizi wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Peter Kiprop, Wakili Mkuu wa Mashtaka Anthony Musyoka na Wakili Mwandamizi wa Mashtaka Peris Ongega walipinga kuahirishwa kwa kesi hiyo wakitupilia mbali madai ya Mackenzie kama njia za kuchelewesha kesi hiyo.

Upande wa DPP ilisema hakuna ubaya kama mahakama itasikiliza ombi lao la dhamana bila uwepo wa Mackenzie, ikieleza kuwa kifungu nambari 50 cha katiba kinaruhusu kusikilizwa kwa kesi yoyote bila mshtakiwa.

Upande wa mashtaka ulisema kuwa Mackenzie ni mfungwa hivyo basi sheria inaagiza atengwe na washukiwa wengine.

Mahakama iliambiwa kuwa Mackenzie amekuwa akiagiza washukiwa wenzake kususia chakula hivyo basi kuibua suala la usalama.

Katika uamuzi wake, hakimu Juma alimtaka afisa wa jela la Shimo la Tewa kufika mahakamani ili kutoa mwanga kuhusu madai kwamba haki za Mackenzie zilikiukwa kama vile kutengwa na wenzake.

Inspekta mkuu wa polisi Raphael Wanjohi pia alitakiwa mahakamani kujibu madai ya utekaji nyara.

Mahama pia iliagiza idara ya kurekebisha tabia kuandaa ripoti za dhamana ili kuiongoza katika kuamua ombi la DPP la kupinga dhamana hiyo.

Juma aliagiza kituo cha kitaifa cha Kupambana na Ugaidi (NCTC) kuandaa ripoti za kisaikolojia kwa kila mmoja wa watuhumiwa.

Mahakama itatoa mwelekeo zaidi mnamo Machi 27, 2024 kesi hiyo itakapotajwa.

Share This Article