Fedha za ufadhili wa wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kiufundi, TVET zitatolewa hivi karibuni.
Huku akisema uzinduzi wa mfumo mpya wa ufadhili wa elimu nchini tayari umefanikiwa, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu amesema Bodi ya Kutoa Mikopo ya Elimu ya Juu, HELB tayari imetoa shilingi bilioni 5.2 kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Vyuo Vikuu mbalimbali nchini.
“Hivi karibuni, tutatoa fedha za ufadhili kwa Vyuo Vikuu na pia Vyuo vya Kiufundi, TVET na kwa wanagenzi punde mchakato wa kushughulikia fedha hizo utakapokamilishwa,” alisema Waziri Machogu wakati akitangaza matokeo ya mtihani wa KCPE wa mwaka 2023 leo Alhamisi.
Waziri aliyasema hayo wakati ambapo wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kiufundi, TVET wamekuwa wakiinyoshea serikali kidole cha lawama kwa kukawia mno kutoa fedha hizo, hali waliohofia ingewachelewesha kufanya mitihani.
Machogu alielezea imani kuwa mfumo mpya wa ufadhili utasaidia kuhakikisha kuwa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kiufundi havikumbwi tena na changamoto za kifedha kama ilivyokuwa siku zilizopita.