Macho kwa Waziri Prof. Ndung’u wakati akitarajiwa kusoma bajeti

Martin Mwanje
2 Min Read
Waziri wa Fedha Prof. Njuguna Ndung'u

Nadhari ya nchi Alhamisi mchana itaelekezwa kwa Waziri wa Fedha Prof. Njuguna Ndung’u.

Prof. Ndung’u anatarajiwa kusoma bajeti ya kwanza ya utawala wa Kenya Kwanza bungeni.

Waziri huyo anatarajiwa kuwasilisha Taarifa ya Bajeti ya trilioni 3.6 ya mwaka 2023/2024 huku bajeti hiyo ikiibua maoni mseto miongoni mwa Wakenya.

Kunao wanaohofia kuwa bajeti hiyo itakuwa chanzo cha mahangaiko zaidi wakati mzigo wa gharama ya maisha tayari umewaelemea.

Hii itakuwa bajeti ya kwanza ya utawala wa Kenya Kwanza ambao umetoa kipaumbele kwa nguzo tano chini ya ajenda yake ya kiuchumi ya kuinua walala hoi.

Bajeti hiyo yenye kima cha trilioni 3.6 itadhamiria kuwianisha suala tete la kulipa madeni na kuhakikisha uthabiti wa uchumi.

Katika mapendekezo ya bajeti hiyo, shilingi trilioni 1.5 zimetengewa matumizi ya kawaida, shilingi bilioni 718 maendeleo wakati shilingi bilioni 986 zikidhamiriwa kulipa madeni ya umma.

Kaunti zitagawana shilingi bilioni 385.

Sekta ya elimu itafurahia mgao mkubwa zaidi wa shilingi bilioni 604 zitakazotumiwa miongoni mwa mambo mengine kuboresha elimu ya sekondari ya chini na kuwaajiri walimu.

Sekta zingine zitakazonufaika pakubwa ni ile ya miundombinu, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na nishati.

Nyanja tano muhimu chini ya ajenda ya serikali hiyo ambazo ni kilimo, biashara ndogo ndogo, nyumba, afya, dijitali na sekta ya ubunifu zinatarajiwa kupata shilingi bilioni 268.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *