Serikali imesema kwamba mipango ya shughuli ya upanzi wa miti kote nchini siku ya Jumatatu itakayoongozwa na Rais Willliam Ruto imekamilika.
Katika taarifa ya pamoja wizara ya mambo ya ndani na wizara ya mazingira na misitu, zimeelezea kwamba machifu wamejukumiwa kugawa miche ya miti kwa wakenya na kuwahamasisha kupanda miche hiyo katika maeneo yao ili kuhakikisha ufanisi wa shughuli hiyo.
Serikali ilitenga siku ya Jumatatu Novemba 13, 2023 kuwa sikukuu ya upanzi wa miti. Wakenya hawatakwenda kazini na badala yake watatumia siku hiyo kupanda miche ya miti.
Wanashauriwa kwenda kwa afisi za machifu zilizo karibu nao kupata miche hiyo ya miti kwa ajili ya upanzi.
Katibu katika wizara ya mambo ya ndani Dr. Raymond Omollo na mwenzake wa wizara ya mazingira na misitu Gitonga Mugambi, wanasema kwamba usambazaji wa miche hiyo hadi kwenye afisi za machifu unaendelea kabla ya kesho.
Kulingana nao maeneo ambako mawaziri, makamishna wa kaunti na magavana hawatafikiakesho, machifu wataongoza shughuli ya upanzi wa miche ya miti.
Lengo la serikali ni kuhakikisha upanzi wa miti bilioni 15 kufikia mwaka 2032.
“Tunaamini kwamba juhudi za pamoja za maafisa wanaowakilisha serikali kuu mashinani na wananchi ni muhimu katika kuafikia lengo la wizara ya mazingira na misitu la upanzi wa miche milioni 150 kufikia mwisho wa siku kesho.” makatibu hao walisema katika taarifa ya pamoja.
Walifafanua kwamba juhudi hizo haziishii tu kwa upanzi bali zinaendelea pia hadi katika kutunza miche hiyo na kuhakikisha inakua.