Mabweni mawili yateketea shuleni Kipsigak kaunti ya Nandi

Marion Bosire
1 Min Read

Moto ambao unadhaniwa kuwashwa kwa kupenda uliteketeza mabweni mawili usiku wa kuamkia leo katika shule ya upili ya wavulana ya Kipsigak katika kaunti ya Nandi.

Taarifa za mwanzo kutoka kwa maafisa wa polisi ziliashiria kwamba hakuna yeyote aliyeumia katika kisa hicho na kwamba wanafunzi wote wako salama.

Wazima moto wa serikali ya kaunti ya Nandi walifika katika shule hiyo wakiwa na magari mawili ya kuzima moto kujaribu kuuzima.

Walinzi wa shule hiyo ya upili wanasemekana kufanikiwa kutibua jaribio la kuchoma mabweni hayo yapata wiki moja iliyopita kisa ambacho bado kilikuwa kinachunguzwa na maafisa wa polisi.

Bweni jingine linasemekana kuchomeka usiku wa kuamkia leo katika shule ya upili ya Mariakani katika kaunti ya Kilifi.

Shirika la msalaba mwekundu linaripoti kwamba moto huo ulizimwa baada ya kuharibu bweni hilo la wanafunzi 150.

Katika shule hiyo vile vile hakukuwa na majeruhi na wahudumu wa shirika la msalaba mwekundu wanatoa usaidizi wa ushauri nasaha na wa aina nyingine shuleni humo.

Website |  + posts
Share This Article