Maafisa wawili wa polisi wakamatwa na mihadarati Moyale

Tom Mathinji
2 Min Read

Maafisa wa polisi wa idara ya uhalifu wa jinai, DCI wamewakamata maafisa wawili wa polisi wa kituo cha polisi cha Moyale, wakiwa na mihadarati aina ya cocaine.

Maafisa hao wa DCI walipata gramu 800 za cocaine kutoka kwa washukiwa hao ambayo ni ya thamani ya shilingi milioni 3.2 katika nyumba ya mmoja wa washukiwa.

Kamanda wa polisi wa kaunti ya Marsabit Patrick Mwakio, alisema kukamatwa kwa washukiwa hao kulitokana na habari kwamba maafisa wawili wa polisi katika kituo hicho walikuwa na mihadarati kinyume cha sheria.

Kulingana na Mwakio, baada ya upekuzi katika nyumba za washukiwa, mihadarati hiyo ilipatikana katika nyumba ya mmoja wa maafisa hao ambao ni wa cheo cha konstebo.

Aidha afisa huyo mkuu wa polisi alisema mihadarati haikupatikana katika nyumba ya mshukiwa wa pili, lakini anawasaidia polisi kwa uchunguzi.

Alisema serikali inajizatiti kushinda vita dhidi ya utumizi na ulanguzi wa dawa za kulevya hapa nchini.

Duru zinasema maafisa hao wa polisi walimkamata mwanamke mmoja raia wa Nigeria aliyekuwa na mihadarati hiyo siku 10 zilizopita, lakini walipokea hongo badala ya kumtia nguvuni mwanamke huyo.

Mshukiwa huyo inasemekana hakuwa na fedha zilizoitishwa na maafisa hao wa polisi, na kwamba alikuwa na  shilingi 300,000 kwa wakati huo.

Maafisa hao ambao sasa wako korokoroni walishikilia mihadarati hiyo ili kumpa muda mwanamke huyo kutafuta fedha zilizosalia ambazo hazijabainishwa ni ngapi.

Mwamamke huyo alitoweka na hakurejea tena na kusababisha maafisa hao wa polisi kuiuza kwa walanguzi wengine walio karibu kabla ya kutiwa nguvuni.

Share This Article