Maafisa wawili wa halmashauri ya ukusanyaji ushuru humu nchini (KRA) wameripotiwa kutoweka baada ya gari lao kusombwa na mafuriko katika eneo la Ramisi kaunti ya Kwale.
Wawili hao wakiwemo, dereva mmoja na afisa mkuu wa halmashauri hiyo walikuwa wakieleka mjini Mombasa kutoka eneo la Lunga Lunga wakati mkasa huo ulipotokea jana jioni.
Kwenye taarifa, kaimu mshirikishi wa eneo la kusini wa KRA Lawrence Siele alisema kwamba halmashauri hiyo tayari imewasiliana na jamaa za maafisa hao wawili na uchunguzi wa kina na oparesheni ya kuwaokoa inayotekelezwa na kundi la vitengo mbali mbali vya serikali inaendelea.
Kadhalika, halmashauri hiyo imesema kwamba usalama wa wafanyakazi wake unasailia kuwa suala linalopewa kipau mbele wanafanya kila jitihada kuwaokoa.
Wakati huo huo, naibu kamishna wa kaunti katika eneo la Lunga Lunga, Joseph Sawe alisema huenda maafisa hao wawili walifariki katika mksasa huo uliotokea jana saa moja usiku.
Kwa mujibu wa Sawe , maafisa hao wawili waliamrishwa na maafisa wa polisi waliopelekwa kulinda eneo hilo kutovuka daraja hilo lakini walikaidi amri hiyo.
Sawe alisema oparesheni ya uokoaji inaendelea ili kupata gari pamoja na maafisa hao.
Kutokana na mkasa huo,Sawe alisema barabra hiyo imetangazwa kuwa haitatumika tena hadi viwango vya maji vipungue.