Maafisa Wakuu watatu wa kaunti ya Nairobi watimuliwa

Tom Mathinji
1 Min Read

Gavana wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja, amewafurusha maafisa wakuu wa kaunti hiyo kutokana na utepetevu kazini.

Kupitia kwa taarifa siku ya Jumatano iliyotiwa Saini na kaimu Katibu na mkuu wa utumishi wa umma wa kaunti hiyo Patrick Analo, watatu hao walichukuliwa hatua hiyo baada ya kudaiwa kuwadhulumu wachuuzi, wafanyabiashara na waendeshaji magari.

Maafisa hao wa kaunti waliotimuliwa ni pamoja na Tony Kimani ambaye ni afisa mkuu wa usalama na uzingatiaji kanuni, Benjamin Omondi mkaguzi mkuu wa kaunti na Carol Njuguna ambaye ni naibu Mkurugenzi wa operesheni.

Kulingana na Analo mabadiliko hayo yanatekelezwa mara moja.

Hivi majuzi serikali ya kaunti ya Nairobi ilijipata pabaya, baada ya maafisa wa kaunti hiyo kuwashambulia wachuuzi wa chakula waliokuwa wakiuza kutumia toroli na kumwaga vyakula hivyo barabarani.

Hatua hiyo iliibua hisia kali kutoka kwa wananchi, huku Gavana Sakaja akiwafidia wachuuzi nao na kuahidi kuwachukilia hatua maafisa husika.

Share This Article