Maafisa wa serikali na umma watapokea nyongeza ya mshahara ya kati ya asilimia 7-10 kati ya mwaka 2023-2024.
Tume ya Mishahara na Marupurupu, SRC inasema malimbikizi ya nyongeza hiyo yatatolewa kuanzia Julai 1, 2023.
Katika mkutano na wanahabari leo Jumatano, mwenyekiti wa SRC Lyn Mengich amedokeza kuwa jumla ya shilingi bilioni 27.1 zimetengwa na Wizara ya Fedha ili kutekeleza nyongeza hiyo katika kipindi hicho.
“Dhamira ya tume ni kuimarisha uwajibikaji, uwazi, usawa, na haki katika utumishi wa umma. Uratibu upya wa marupurupu si tu unalenga kufikia uimara wa kifedha bali pia unasisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa utumishi wa umma unabaki kuwa na gharama nafuu,” alisema Mengich.
Walimu ndio watakaonufaika zaidi na nyongeza hiyo baada ya kutengewa kitita cha jumla ya shilingi bilioni 9.5 wakifuatwa na polisi na wanajeshi waliotengewa jumla ya shilingi bilioni 4.5. Wafanyakazi wa kaunti wametengewa shilingi bilioni 4.07, watumishi wa umma shilingi bilioni 1.8 huku maafisa wengine wa umma wakitengewa shilingi milioni 745.6. Maafisa wa idara ya mahakama wametengewa nyongeza ya jumla ya shilingi milioni 305.2 wakati wale wa bunge wakitengewa shilingi milioni 78.8. Maafisa wakuu wa serikali wametengewa nyongeza ya jumla ya shilingi milioni 126.9.
Mengich anasema katika mapitio yao ya awamu ya pili, marupurupu manne yalifutiliwa mbali baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kina. Nayo ni marupurupu ya kuhudhuria warsha, marupurupu ya vikao vya ndani vya taasisi, marupurupu ya vikao vya ndani vya jopokazi, pamoja na marupurupu ya kujikimu kwa siku kwa safari za ndani.
Marupurupu ya kujikimu kwa siku kwa safari za nje ya nchi yatabaki kama yalivyo, isipokuwa kwa marekebisho kadhaa kulingana na viwango vilivyosahihishwa kwa nchi kadhaa.
Makusudi ya SRC ni kuokoa mabilioni ya fedha zinazotumiwa katika ulipaji wa marupurupu na kukuza sekta ya utumishi wa umma iliyo na ufanisi na usawa ili kuafikia matokeo bora ya utendakazi.