Katibu katika wizara ya usalama wa taifa Dkt. Raymond Omollo, amesema maafisa wote wa polisi walipata nyongeza ya mshahara kuanzia mwezi Julai 1, 2024.
Kulingana na Dkt. Omollo, katika awamu ya kwanza maafisa wa cheo cha konstebo, walipata nyongeza ya mshahara ya asilimia 40, huku walio katika vyeo vya juu wakipata nyongeza ya asilimia 3.
Kupitia kwa taarifa leo Jumatano, Katibu huyo alisema kuanzia mwezi Septemba mwaka huu, maafisa wa huduma za magereza na wale wa huduma za vijana kwa taifa NYS, wataanza kupokea nyongeza ya mshahara.
Alisema hatua hiyo ni kuambatana na agizo la Rais la kutekelezwa mapendekezo ya jopokazi lililoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu David Maraga, katika taasisi hizo.
“Mchakato huo wa mageuzi utachukua muda wa miaka minne, kuanzia mwaka 2024 hadi 2028,” alisema Dkt. Omollo.
Ili kuhakikisha utekelezwaji wa mageuzi hayo unafaulu, Dkt. Omollo alisema wizara hiyo imebuni kamati za kiufundi kuhusu mikakati ya sheria na sera katika huduma hizo tatu.
“Kamati za mageuzi zimebuniwa katika huduma ya taifa ya polisi, huduma ya magereza na huduma ya vijana kwa taifa, kushirikisha utekelezwaji wa mageuzi hayo,” aliongeza Dkt. Omollo.