Maafisa wa polisi waliomjeruhi mchuuzi kuzuiliwa kwa siku 15

Tom Mathinji
1 Min Read
Maafisa wa polisi waliohusishwa na kisa cha kumpiga risasi mchuuzi kuzuiliwa kwa siku 15.

Mahakama moja ya Nairobi, imeagiza Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), kuwazuilia kwa siku 15 maafisa wawili wa polisi waliohusishwa na kisa cha kumpiga risasi mchuuzi wakati wa maandamano Jijini Nairobi Jumanne iliyopita.

Konstebo Masinde Klinzy Barasa, aliyetambuliwa kuwa alifyetua risasi na Duncan Kiprono, aliyekuwa katika eneo la mkasa, walifikishwa katika mahakama ya Milimani siku ya Alhamisi.

Mahakama iliagiza swala hilo litajwe Julai 3,2025, kuthbitisha mchakato wa uchunguzi wa kesi hiyo.

Kisa hicho kilichotokea kwenye barabara ya Tom Mboya na kunaswa kwa video, kimesababisha hamaki miongoni mwa umma, huku miito ya maafisa hao kuchukuliwa hatua za kisheria ikisheheni.

Mchuuzi huyo alipigwa risasi wakati wa maandamano dhidi ya ukatili wa polisi na mauaji ya hivi majuzi ya mwanablogu Albert Ojwang akiwa mikononi mwa polisi.

Mwathiriwa huyo mwenye umri wa miaka 22 Boniface Mwangi Kariuki, alipelekwa katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta ambako anaendelea kupokea matibabu.

Website |  + posts
Share This Article