Taifa hili linapojiandaa kwa msimu wa sherehe, maafisa wote wa polisi walio likizoni wameagizwa kurejea kazini.
Kupitia kwa taarifa Inspekta Jenerali wa polisi Japhet Koome, amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha usalama kote nchini.
Koome alitoa wito kwa abiria, waendeshaji magari, waendeshaji baiskeli na Kwa wanaotembea kwa miguu, kuzingatia sheria za trafiki ili kufanya msimu huu wa sherehe kuwa salama kwa wote.
“Nawahimiza wanaotembea kwa miguu, waendeshaji baiskeli, Pikipiki, waendeshaji magari na abiria, kuzingatia sheria za trafiki ili tufanikishe msimu huu wa sherehe,” alisema Koome.
Kulingana na Koome, kutakuwa na msongamano mkubwa wa magari kutokana na pilkapilka za wakenya wanasafiri katika sehemu mbali mbali za nchi.
Aidha Inspekta Jenerali huyo alisema huduma ya taifa ya polisi inaunga mkono misako inayotekelezwa na halmashauri ya uchukuzi na usalama barabarani-NTSA, na tume ya maadili na kukabiliana na ufisadi EACC, ili kuhakikisha usalama unadumishwa barabarani.
Koome pia alitoa wito kwa wakenya kuendelea kuwa waangalifu, akiwataka kuripoti visa vyovyote vya uhalifu katika vituo vya polisi vilivyoko karibu, ama pia kuputia Nambari za simu 999,112,911 na 0800 722 203.