Maafisa wa NTSA kurejeshwa barabarani

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen amesema kwamba yeye na Waziri wa Usalama wa Taifa Kithure Kindiki wamekubaliana kutafuta kufutiliwa mbali kwa agizo la kuwaondoa barabarani maafisa wa Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama Barabarani, NTSA.

Maafisa wa NTSA waliondolewa kwenye barabara za humu nchini yapata miaka sita iliyopita kufuatia agizo la Rais wa wakati huo Uhuru Kenyatta.

Rais Uhuru wakati huo alielekeza kwamba utekelezaji wa sheria za trafiki uachiwe idara ya trafiki katika huduma ya taifa ya polisi.

Sasa Waziri Murkomen ambaye yuko nchini Rwanda kwa mkutano na mwenzake wa nchi hiyo kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano wa usafiri kati ya nchi hizi mbili anasema matukio ya ajali nchini yamechochea kurejeshwa kwa maafisa wa NTSA.

Huku akitoa risala za rambirambi kwa ndugu na marafiki wa waathiriwa wa ajali za hivi majuzi nchini, Murkomen aliorodhesha hatua ambazo wamepiga katika kuimarisha usalama barabarani kama wizara.

Alisema sheria zimeundwa za kushughulikia wanaoendesha magari wakiwa walevi na uendeshaji wa magari mazito ya usafirishaji bidhaa na zitawasilishwa kwa kamati husika ya bunge mwanzoni mwa mwezi ujao.

Kuhusu magari ya usafirishaji wa wanafunzi, Murkomen alisema wameweka masharti mapya kama vile kuwekwa kwa vifaa vya kufuatilia magari hayo, kuwekwa kwa vifaa vya kulinda wanafunzi wanapokuwa kwenye magari hayo pamoja na kila gari kama hilo kuwa na mhudumu wa kuhakikisha usalama wa wanafunzi kando na mwendeshaji.

Chini ya mpango wa ushirikiano kati ya NTSA na polisi wa trafiki wa kuhakikisha usalama barabarani unaotarajiwa kuanza hivi karibuni, madereva watasailiwa upya.

Share This Article